Katika kuelekea sikukuu za X-Mass na Mwaka Mpya, ambapo wananchi wenye imani ya kikristo na hata madhehebu mengine hutumia muda huo kwenda kuabudu pamoja na muendelezo wa sherehe hizo kwenye maeneo mengine ya starehe. Uzoefu unaonyesha kwamba sikukuu hizo za mwisho wa mwaka huambatana na vitendo vinavyohatarisha usalama wa raia na mali ambapo baadhi ya watu kutumia vilevi kupita kiasi, kujipatia kipato kwa njia ya udanganyifu (utapeli), wizi, unyang’anyi pamoja na uendeshaji wa vyombo vya moto bila kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.

Kufutia matishio hayo, Jeshi la Polisi nchini, limejipanga kikamilifu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba wananchi wanasherehekea sikukuu hizo kwa amani na utulivu bila ya kuwepo vitendo vyovyote vya uhalifu. Ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.

 

Aidha, Jeshi la Polisi linatoa tahadhari kwa wananchi wote kuwa makini na kuchukua hatua stahiki za haraka kwa kutoa taarifa kupitia namba za makamanda wa Polisi wa Mikoa na namba za bure 111 na 112 pindi wanapoona viashiria vyovyote vya uhalifu katika maeneo mbalimbali na watokapo kwenye makazi yao wasiache nyumba wazi ama bila mtu na badala yake watoe taarifa kwa majirani zao.

Pia, Jeshi la Polisi linawatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara, kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani na hasa kwa madereva wa magari na pikipiki, kuepuka kwenda mwendo kasi na kutumia vilevi wawapo kazini.

Wamiliki wa kumbi za starehe wazingatie uhalali na matumizi ya kumbi zao katika uingizaji wa watu kulingana na uwezo wa kumbi hizo, badala ya kuendekeza tamaa ya fedha kwa kujaza watu kupita kiasi. vilevile, wazazi wawe makini na watoto wao ili kuepuka upotevu watoto, ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara juu yao.

Hali kadhalika, Wamiliki wa maduka makubwa tunawakumbusha kufunga kamera za cctv ili kurekodi mienendo ya watu wanaoingia na kutoka katika maduka yao kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali na kuweza kubaini uhalifu na wahalifu kwa haraka.

Mwisho, napenda kuwahakikishia wananchi kwamba, Jeshi la Polisi linatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria za nchi na hivyo halitawajibika kumwonea huruma ama upendeleo mtu yeyote atakayeenda kinyume na sheria.

Imetolewa na:-

Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Advera John Bulimba,

Msemaji wa Jeshi la Polisi,

Makao Makuu ya Polisi.